Na mwandishi wetu;
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Geita, Evarist Gervas, amewataka
wananchi wa Kata ya Busanda, Jimbo la Busanda, kujitokeza kwa wingi kupiga kura
Oktoba 29, akisisitiza kuwa kura zao ni muhimu kwa kuendeleza maendeleo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni katika kata hiyo, leo Septemba 29,2025, Gervas amesema kuwa mtu yeyote atakayewashawishi wananchi wasipige kura siku hiyo ni “adui wa maendeleo” na wanapaswa kuepukwa.
“Ndugu zangu wa Busanda, atakayewambia msipige kura Oktoba 29, huyo si rafiki wa maendeleo. Ni mtu wa kumuepuka kabisa. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mengi makubwa ndani ya Mkoa wetu, ili aendelee, tushiriki kupiga kura kwa CCM na wagombea wote wa ccm,” amesema Evarist.
Aidha, ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika Jimbo la Busanda na Mkoa wa Geita kwa ujumla yanadhihirisha dhamira ya kweli ya CCM na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Evalist amehitimisha kwa kutoa wito
kwa wanachama wa CCM na wananchi wote kwa ujumla kuhakikisha wanajitokeza kwa
wingi kupiga kura ili kuendeleza kasi ya maendeleo nchini.






0 Comments