Na
Victor Bariety, Geita;
Septemba 2025
Mwenge
wa Uhuru Kitaifa 2025 umeendelea kutoa heshima kubwa kwa Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Geita, baada ya kuzindua rasmi mradi wa
boksi kalavati katika barabara ya Kharumwa–Nyijundu, wilayani Nyang’wale.
Uzinduzi
huo umeweka historia, kwani ni mara ya tatu mfululizo ndani ya wiki moja miradi
ya TARURA Geita kuibua pongezi kutoka kwa kiongozi wa mbio hizo, Ndg. Ismail
Ali Ussi. Awali Mwenge huo ulipita na kuridhishwa na miradi ya barabara ya
Nzera (Wilaya ya Geita) na Kasco (Manispaa ya Geita), na sasa umehitimisha na
mradi wa Nyang’wale.
Pongezi
kutoka kwa kiongozi wa Mwenge
Akitoa kauli yake baada ya ukaguzi, Ndg. Ussi alisisitiza kuwa Geita imeonesha mfano wa kuigwa kitaifa.
“Nimepitia
miradi hii kwa makini, nimeona nyaraka na kazi iliyofanyika. Hakuna dosari. Hii
ndiyo inayoonesha fedha za wananchi zinatumika ipasavyo. Hongereni sana
TARURA,” amesema na kisha kutangaza uzinduzi rasmi wa mradi huo.
Maelezo ya kitaalamu
Kwa
mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyang’wale, Mhandisi John Msita, mradi huo
uligharimu shilingi 579,680,000.00, ukifadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mwaka wa
fedha 2023/2024.
Kazi
zilizotekelezwa zilihusisha ujenzi wa boksi kalavati mbili za zege, kalavati
ndogo nane, pamoja na matengenezo ya kilomita moja ya barabara ya changarawe.
Kazi ilianza Juni 18, 2024 na kukamilika Aprili 14, 2025 na ilifanywa na
kampuni ya D4N Company Ltd kutoka Kahama.
Mhandisi
Msita aliongeza kuwa mradi huo umeondoa usumbufu mkubwa uliokuwa ukiwalazimisha
wananchi kuzunguka umbali wa kilomita 98 kufika makao makuu ya Wilaya ya
Nyang’wale, Kharumwa. Kwa sasa umbali huo umepungua na kufikia kilomita 90
pekee.
Manufaa kwa wananchi
Wananchi wa Kijiji cha Bukungu, wakiongozwa na mwenyekiti wao Hadija Samson, walieleza jinsi walivyokuwa wakiteseka kabla ya mradi huo.“Zamani tulivuka kwenye daraja la miti, tena kwa kulipia ada ya shilingi 500 kwa miguu na shilingi 5,000 kwa pikipiki. Wengi walihatarisha maisha yao wakati wa mafuriko. Lakini leo tuna daraja imara la zege. Tunamshukuru Rais Samia, TARURA na viongozi wetu wa CCM kwa kazi kubwa,” amesema Hadija huku akishangiliwa.
Ujumbe wa amani na maendeleoZaidi ya kuzungumzia mradi huo, Ndg. Ussi alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi juu ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Kumchagua
Rais Samia ni kuchagua maendeleo—barabara, madaraja, maji, umeme na afya.
Lazima tulinde amani ili vizazi vijavyo vibaki na miradi hii,” amesitiza.
Geita
yaandika ukurasa mpya
Kwa mara ya kwanza, miradi mitatu mfululizo ya TARURA katika mkoa mmoja imepata sifa ya kiwango cha juu mbele ya Mwenge wa Uhuru. Hali hii imeweka rekodi mpya Geita, tofauti na hali ya miaka ya nyuma katika maeneo mbalimbali nchini ambapo baadhi ya miradi haikuzinduliwa kwa kuwa haikukidhi viwango.
Wananchi
sasa wanaona ushahidi wa kodi zao zikigeuka miundombinu ya maana, ikirahisisha
biashara, usafirishaji na maisha ya kila siku. TARURA Geita imejipambanua kama
kielelezo cha uwajibikaji na nidhamu katika utekelezaji wa miradi ya barabara
nchini.
Hata
hivyo, Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 bado unaendelea mkoani Geita ukizindua
miradi mbalimbali ya maendeleo iliyo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Hadi sasa, hakuna mradi uliokosolewa
kwa kujengwa chini ya kiwango, lakini pale unapoifikia miradi ya TARURA,
mkimbiza Mwenge amekuwa akimwaga sifa nyingi zaidi. Hali hiyo imeongeza morali
na uadilifu kwa watumishi wa TARURA kuona mchango wao katika taifa unatambulika,
kana kwamba ni tuzo ya kufanya vizuri.
Licha
ya kuwepo miradi ya sekta nyingine kama afya na maji, miradi ya TARURA imekuwa
kivutio kikubwa kwa kiongozi wa Mwenge. Leo Mwenge unaendelea kukimbizwa katika
Wilaya ya Mbogwe ukizindua miradi mbalimbali, na kwa kuwa TARURA tayari
wameanza vizuri, wafanyakazi wake wanaamini hata miradi iliyopo Mbogwe, Bukombe
na Chato nayo itafunika kwa ubora. Hayo ni kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Mkoa
wa Geita, Mhandisi David Msechu.
0 Comments