TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

SAMIA SULUHU HASSAN: KIONGOZI WA KUTENDA, AHADI ZIPO UPINZANI

Na Victor Bariety;

Tanzania imebahatika kuwa na viongozi waliokuwa watu wa vitendo. Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alijulikana kwa kauli yake ya “Hapa Kazi Tu”, na alipoahidi hakusubiri muda mrefu kutekeleza. Leo hii, Rais Samia Suluhu Hassan ameendeleza misingi hiyo ya uongozi wa kutenda, huku akionesha mfano wa kiongozi anayesema na kutenda pasipo kusita.

 


Ni mara ngapi tumewaona wanasiasa wengi wakiomba nafasi ya uongozi kwa kuahidi mambo, lakini wachache sana wamekuwa tayari kutekeleza kabla hata ya kupewa nafasi nyingine? Ndipo swali linapojitokeza: “Tumpate wapi kiongozi anayesema na kutenda kama Mama Samia?”


Alivyotenda Katika Afya

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Serikali ya Rais Samia imeacha alama kubwa kwenye sekta ya afya. Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2023, idadi ya vituo vya afya nchini imeongezeka kutoka 8,458 mwaka 2020 hadi 9,826 mwaka 2024. Hospitali zenye huduma za dharura (EMD) zimeongezeka kutoka 7 mwaka 2020 hadi 113 mwaka 2024, huku huduma za wajawazito na watoto (CEmONC) zikiongezeka kutoka 340 hadi 523.

 

Aidha, uwezo wa vitanda hospitalini umeongezeka kutoka 84,162 mwaka 2020 hadi 123,769 mwaka 2024 — ongezeko la zaidi ya vitanda 39,000. Vifaa tiba vya kisasa kama CT-Scan, MRI na mashine za dialysis pia vimeongezeka, kutoka mashine 60 mwaka 2021/22 hadi 137 mwaka 2024/25, huku hospitali zinazotoa huduma hiyo zikiongezeka kutoka 6 hadi 15.


Mwananchi mmoja wa Tabora anaeleza:

“Huduma zimekaribia, wagonjwa hawalazimiki tena kusafiri mbali. Hii ni kazi inayoguswa kwa macho na si ahadi tupu.”

Alivyotenda Katika Elimu

Sekta ya elimu nayo imepata msukumo mkubwa. Ripoti ya Wizara ya Elimu ya mwaka 2025 inaonyesha kuwa ndani ya kipindi cha miaka miwili pekee, Serikali imetumia zaidi ya Shilingi trilioni 1.29 kujenga miundombinu ya elimu, ikiwemo shule 486 za sekondari mpya na madarasa 21,990, pamoja na nyumba za walimu, hosteli na maabara.

 


Zaidi ya hapo, Rais Samia amezindua mradi wa ujenzi wa shule 103 za sekondari za ufundi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 41.6, ili kuwaandaa vijana kushindana kwenye soko la ajira.

Katika upande wa rasilimali watu, kati ya mwaka wa fedha 2020/21 na 2022/23, Serikali imeajiri takribani walimu 29,879, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa walimu katika shule za umma. Hata hivyo, ripoti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (PO-RALG) inaonyesha kuwa bado kuna upungufu wa walimu 271,025 katika ngazi zote za elimu.

 




Mwalimu mmoja wa sekondari Tabora anasema:

“Walimu wapya waliokuja wametusaidia sana. Madarasa hayana msongamano kama zamani, na wanafunzi wanapata msaada wa karibu zaidi.”

 

Kauli Yake Tabora

Akiwa Tabora, katika viwanja vya Tarafa ya Uyui, kata ya Ilolanguru, mgombea huyo wa CCM alisisitiza kwamba endapo ataendelea kuaminiwa kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, ndani ya siku 100 Serikali yake itaajiri watumishi 5,000 wa kada ya afya na 7,000 wa kada ya elimu.

“Ndani ya siku 100 katika sekta ya afya tutaajiri Watumishi 5,000 ambao pia bila shaka watafika na hapa, lakini vilevile pia katika sekta ya elimu takribani Watumishi 7,000 tutaajiri na hapa pia watafika,” alisema Dkt. Samia, akipokelewa kwa shangwe kubwa.

 

Kutokana na ukubwa wa eneo la Tabora na changamoto za upatikanaji huduma, ameahidi kujenga vituo vipya vya afya na kusaidia kumalizia miradi ya afya iliyoanzishwa na wananchi.

 

Mwanafunzi mmoja wa Uyui alisema:

 “Tumeanza kuona walimu wa masomo ya sayansi wakija shuleni kwetu. Hii inatupa matumaini kwamba hata ahadi mpya zitatekelezwa.”

 

Hitimisho

Kwa kuangalia yaliyotekelezwa na anayoahidi, picha inajengeka wazi: Rais Samia si kiongozi wa maneno pekee, bali wa vitendo vinavyoonekana. Ameajiri walimu, ameongeza vitanda hospitalini, ameongeza vituo vya afya, ameanzisha shule za ufundi, na sasa anaomba ridhaa kuendeleza pale alipofanikisha.

Kwa Watanzania, swali la msingi linabaki: Je, tutamwacha kiongozi wa kutenda na kumchagua mwenye ahadi pekee?

 

Mwisho

Imeandaliwa na Victor Bariety – 0757 856 284

 

Post a Comment

0 Comments