TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

TANZANIA YAZIDI KUPAA: KUTOKA NCHI MASKINI HADI UCHUMI WA KATI


Na Victor Bariety;

 

Picha:Katibu mkuuWizara ya fedha 

Tanzania imeorodheshwa na Kamati ya Sera za Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UN) miongoni mwa nchi zinazotazamiwa kufuzu kutoka kundi la nchi maskini zaidi (Least Developed Countries – LDCs) kwenda kwenye kundi la nchi zinazoendelea.

Tangazo hilo lilitolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati wa Mkutano wa Awali wa tathmini ya UN kupitia Shirika lake la Biashara na Maendeleo (UNCTAD).

Dkt. Mwamba alisema kuwa hatua hiyo imetokana na Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Ukuaji wa uchumi umekuwa wa wastani wa asilimia 6.2 kati ya mwaka 2000 na 2024.

 

 “Pato la mtu kwa mwaka limeongezeka kutoka dola 453 mwaka 2000 hadi dola 1,277 mwaka 2023, kiwango cha umasikini uliokithiri kimepungua kutoka asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2024, kutokana na sera thabiti za kifedha na ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi,” amesema Dkt. Mwamba.

Aidha, aliongeza kuwa mfumuko wa bei umeendelea kudhibitiwa na kubaki katika tarakimu moja, hali iliyoongeza uthabiti wa uchumi na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi. 

Miradi Mikubwa ya Kimkakati

Dkt. Mwamba alitaja miradi kadhaa yenye mchango mkubwa 

Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP),

Reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), 

Maboresho makubwa katika sekta ya elimu na afya.

Amesema miradi hii imeongeza tija, ajira na nafasi za uwekezaji, hivyo kuimarisha vigezo vinavyohitajika kuondoa Tanzania kwenye kundi la nchi maskini.


Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Mhe. Shigeki Komatsubara, alisema Umoja wa Mataifa uko tayari kuisaidia Tanzania kufanikisha safari hii kwa urahisi zaidi, kwa kuwa mchakato wa tathmini ni shirikishi na unazingatia maoni ya wananchi wa rika zote.


Picha: Mwakilishi UNDP

Mtazamo wa Wadau

Mkutano huo ulijumuisha wadau kutoka Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, mashirika ya maendeleo na taasisi za elimu.

Wadau walitoa maoni kwamba hatua ya Tanzania kufuzu kutoka kundi la LDCs ni kielelezo cha uthabiti wa sera na mshikamano wa wananchi. Hata hivyo walisisitiza mambo yafuatayo:


Picha: Wadau wa maendeleo wakifuatilia mjadala kwa makini

1. Kuwekeza zaidi kwenye kilimo kwa kuongeza thamani kupitia usindikaji ili kuongeza ajira vijijini.

2. Ajira za vijana zipewe kipaumbele kwa kukuza sekta ya teknolojia na biashara ndogo.

3. Uendelevu wa miradi mikubwa (nishati na reli) uhakikishwe kwa matokeo ya muda mrefu.

4. Elimu na afya viendelee kuboreshwa ili kujenga nguvu kazi yenye ujuzi.

5. Pengo la kijinsia lipunguzwe kwa kuwezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi.

 

Picha: Baadhi ya wadau wa maendeleo wakifuatilia mjadala kwa makini

Changamoto Zinazobaki

Ajira kwa vijana bado ni changamoto kubwa.

Uchumi unategemea sana sekta ya kilimo na madini.

Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri uzalishaji na usalama wa chakula.

 

Hitimisho

Safari ya Tanzania kutoka kwenye kundi la nchi maskini zaidi kuelekea uchumi wa kati ni simulizi ya matumaini na uthabiti. Ni safari iliyojaa mafanikio ya sera, nidhamu ya kifedha, uwekezaji katika miradi mikubwa na mshirikiano wa kimataifa.

Hata hivyo, kama walivyosisitiza wadau, kuhusu ajira, kilimo na elimu bado kunahitaji msukumo zaidi ili mafanikio haya yawe ya kudumu na kugusa maisha ya kila Mtanzania.

Kwa hatua hii, Tanzania imeweka msingi wa taifa imara na lenye matumaini makubwa ya maendeleo jumuishi kwa wote.

Mwisho 

Imeandaliwa na Victor Bariety

0757-856284

 

Post a Comment

0 Comments