Na Victor Bariety;
Shirika la Human Rights Watch (HRW)
mnamo Septemba 29, 2025, lilitoa ripoti yenye madai mazito kuhusu hali ya haki
za binadamu nchini Tanzania. Ripoti hiyo ilidai kupungua kwa nafasi ya kiraia,
ukandamizaji wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025, pamoja na vitendo vya
utekaji nyara. Hata hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia Msemaji wake, Gerson
Msigwa, imekanusha vikali madai hayo, ikisema yana upotoshaji na hayakuwiana na
hali halisi ya nchi.
Kwa mtazamo wa kitaaluma, ni muhimu kuyachambua madai hayo kwa mizani ya hoja, ushahidi wa kisheria na kisiasa, na matukio halisi yaliyoshuhudiwa.
1. Je, Nafasi ya Kiraia Imefungwa?
Ripoti ya HRW imedai nafasi ya kiraia imezidi kudorora. Hata hivyo, hali halisi ya Tanzania inathibitisha uwepo wa mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari binafsi, na harakati za kijamii zinazofanya kazi. Kwa mfano, vyombo vya habari vya binafsi na vya kijamii vinaendelea kuripoti masuala ya kisiasa na kijamii, na mijadala ya wazi imekuwa ikionekana kwenye majukwaa ya redio na televisheni za ndani.
Aidha, mikutano ya hadhara ya kisiasa imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali, hususan vyama vinavyoshiriki uchaguzi huu, kama vile ACT-Wazalendo, CUF,Chama Makini , na vingine. Ushiriki huu unaonesha kwamba anga ya kiraia bado ipo, tofauti na taswira ya kufungwa kabisa iliyotolewa na HRW.
Rais Samia Suluhu Hassan pia amesisitiza kwamba "Tanzania inabaki kuwa taifa lenye nafasi ya kiraia, ambapo wananchi wana uhuru wa kushiriki katika siasa kwa misingi ya sheria na amani" (Rais Samia Suluhu Hassan, Hotuba, Agosti 2025).
2. Ushiriki wa Vyama Vya Siasa
Moja ya hoja kuu ya HRW ni kwamba uchaguzi mkuu wa 2025 unakosa usawa wa kisiasa. Hata hivyo, ukweli ni kwamba vyama vilivyosajiliwa na ambavyo havikujiondoa, vinaendelea kushiriki kikamilifu mchakato wa uchaguzi. Sheria ya Uchaguzi ya Rais, Bunge na Madiwani (Na. 1 ya 2024) imeweka taratibu za uwanja sawa—ikiwemo masharti ya fedha za uchaguzi, nafasi ya Tume Huru ya Uchaguzi, na usawa wa vyama katika kufanikisha kampeni.
Ni kweli chama kikuu cha upinzani, Chadema, kilitangaza kujiondoa kwenye uchaguzi huu, lakini vyama vingine vimeendelea kushiriki kikamilifu. Hivyo madai kwamba hakuna ushindani wa kisiasa hayana mashiko kamili, kwani ushindani bado upo kupitia vyama vingine vinavyoshiriki.
3. Tuhuma za Utekaji Nyara
Ripoti ya HRW pia imetaja vitendo vya utekaji nyara. Serikali kwa upande wake imesisitiza kwamba mamlaka za usalama hazina sera ya kuvunja haki za raia na kwamba kila tukio linalohusiana na jinai linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Tukio linapojitokeza, vyombo kama Polisi na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora huchunguza kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Ni upotoshaji kuyahusisha moja kwa moja na sera ya Serikali bila ushahidi wa moja kwa moja.
Mfano halisi: Mnamo Juni 6, 2025, Sheikh Zuberi Said Nkokoo, kiongozi wa Kiislamu kutoka Singida, alidaiwa kutekwa nyara. Hata hivyo, uchunguzi wa Polisi ulionyesha kwamba Sheikh Nkokoo alijitengenezea tukio la kutekwa nyara kutokana na deni la takribani Tsh 512 milioni. Polisi walithibitisha kwamba alikuwa amejificha kwa hiari yake ili kuepuka madeni (Chanzo: The Citizen, Juni 19, 2025).
4. Wajibu wa Tanzania katika Mikataba ya Kimataifa
Tanzania imeridhia mikataba kadhaa ya kimataifa ya haki za binadamu, ikiwemo:
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR, 1966)
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (ACHPR, 1981)
Kwa kufanya hivyo, nchi imeweka wazi dhamira yake ya kulinda na kutekeleza haki hizo (UN Treaty Collection, 2025).
Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (Ibara ya 12 hadi 24) inatamka bayana haki za msingi za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, uhuru wa mtu binafsi, na usawa mbele ya sheria. Kwa mfano, Ibara ya 12(2) inasema: "Kila mtu anastahili heshima ya kutambulika na kuthaminiwa utu wake."
Hakuna nchi isiyo na changamoto. Tanzania nayo inakabiliwa na changamoto zake, hususan katika maeneo ya kisiasa na kijamii. Hata hivyo, Serikali imeonesha dalili za kujitahidi kupitia:
Mageuzi ya kisheria
Uanzishwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi
Mjadala unaoendelea kuhusu Katiba mpya
Hii ni ishara ya mwamko wa ndani wa kusahihisha kasoro badala ya kuzikwepa.
Hitimisho
Ripoti ya HRW imeibua hoja zinazostahili mjadala. Lakini taswira kwamba Tanzania ni nchi iliyofunga anga ya kisiasa si sahihi kwa kiwango kilichotajwa. Ushiriki wa vyama mbalimbali katika uchaguzi, kuendelea kwa mijadala ya wazi kwenye vyombo vya habari, na misingi ya Katiba vinathibitisha kwamba bado kuna nafasi za kiraia na kisiasa.
Njia bora mbele ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya habari, na mashirika ya haki za binadamu, kwa misingi ya ukweli, uwazi, na mawasiliano ya moja kwa moja. Tanzania, kama taifa huru, inabeba jukumu la kulinda heshima yake kimataifa huku ikibaki mwaminifu katika kulinda haki za watu wake.
Imeandaliwa na: Victor Bariety
Simu: 0757‑856284

0 Comments