TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

KANISA LA ANGLIKANA LALAANI VIKALI VITENDO VYA UKATILI KWA WATOTO

Mhashamu Baba Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza  Rt. Rev.Zephania Amosi Ntuza (katikati) akiongoza ibada maalumu  kwenye kanisa la Anglikana Kristo Mfalme Geita. Kulia ni Mchungaji Andrew Kashilimu na kushoto ni Mchungaji Kanoni Kasisi Rodgers Kashimba.

 Na Samwel Masunzu,Geita

Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza limelaani vikali vitendo vya ukatili kwa watoto ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wazazi na walezi na kusababisha  watoto  kukosa  haki zao ikiwemo haki ya kupata elimu na kuishi.

Hayo yameelezwa na Mhashamu Baba Askofu wa kanisa la Angilkana Dayosisi ya Victoria Nyanza Rev. Zephania  Amosi Ntuza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kanisa jipya la Anglikana Kristo Mfalme Mjini Geita pamoja na kumuweka wakfu kiongozi wa walei wa kanisa hilo ndugu Godwin Busugulu.

Baba Askofu Ntuza amesema kanisa linalaani vikali vitendo hivyo ikiwa ni baada ya mtoto wa darasa la saba mkoani Geita kushindwa kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu ya msingi baada ya mama yake kumchoma moto mikono yake ikidaiwa kuwa mtoto huyo ameiba kiasi cha shilingi elfu thelathini tukio ambalo kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita ACP Safia Jongo amekiri kutokea kwenye mkoa huo

Amesema pia kanisa linaiomba serikali kuendelea kuchukua hatua kali kwa wazazi ama walezi wanaowafanyia watoto wao vitendo vya ukatili kwa makusudi

“sisi kama kanisa, tumesikitishwa sana na kitendo hicho pamoja na matukio mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye jamii ya kuwakatili watoto, na ombi letu kwa serikali ni kuona hatua zinachukuliwa kwa wahusika ili kuwanusuru watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo viovu”

Mhashamu Baba Askofu akimuweka wakfu kiongozi wa walei Godwin Busugulu

Mchugaji Kanoni Joseph Samwel Kitwe ambaye ni mchungaji kiongozi wa kanisa la Anglikana Kristo Mfalme Geita amesema kanisa litaendelea kutetea wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na kusisitiza kauli ya Baba Askofu ya wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kueleza wanayofanyiwa badala ya kuendelea kukaa kimya ilihali vitendo hivyo vikiendelea kuwaumiza.

Mchungaji kiongozi wa kanisa la Kristo Mfalme Kanoni Joseph Samwel Kitwe akieleza jinsi atakavyotekeleza maelekezo ya Mhashamu Baba Askofu.

Awali mwenyekiti wa kamati ya mipango na maendeleo katika kanisa la Anglikana Kristo Mfalme James Mtalitinya  pamoja  na mmoja wa waumini wa kanisa hilo Bi. Joyce Seka    wamesema kutokana na kauli ya Baba Askofu, wataendelea kusimamia nafasi zao kama wazazi huku wakieleza kuwa moja ya sababu ya uwepo wa watoto wa mitaani ni pamoja na kukosekana kwa misingi ya malezi bora kutoka kwa wazazi.

Mhashamu Baba Askofu akitoa kipaimala.


Katibu wa kanisa la Anglikana Kristo Mfalme Geita na katibu wa Parishi ndugu  Amani Ndaba amesema ujenzi wa kanisa hilo ulianza mwaka 2020 kwa michango ya waumini wa kanisa hilo na ujenzi utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.40 hadi kukamilika kwake na kwa sasa ujenzi huo umeshagharimu kiasi cha shilingi milioni 204 na  ukiwa umefikia asilimia 20. 

MWISHO.

Post a Comment

2 Comments

  1. Mungu WA mbiguni asikie maombi ya watumishi wake. Ujenzi uendelee sana na, ukatili ukomeshwe

    ReplyDelete
  2. Asanteni sana kuleta njia hii ya taarifa za Anglikana Geita

    ReplyDelete