TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

MKATABA WA LISHE NA UZAZI WA MPANGO UNAVYOWEZA KUTOKOMEZA TATIZO LA UDUMAVU KWA WATOTO MKOANI GEITA

Martine Shigela Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela.

Na Salum Maige, Geita
Inaelezwa Kwamba Kuboresha Lishe ni Msingi Katika Kufanikisha Malengo Endelevu ya Maendeleo kwenye Taifa lolote hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Nchini Tanzania Hatua hiyo inakabiliwa na Changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uwepo wa Utapiamlo sugu(Udumavu)unaodhoofisha Maendeleo katika Uhakika wa Chakula,Uboreshaji wa Elimu,na Afya bora ya mama na Mtoto.

Kwa Mujibu wa Watalaamu wa Masuala ya Lishe ni Kwamba Lishe Duni ndio sababu kubwa ya Vifo vya watoto chini ya umri wa Miaka Mitano nchini Tanzania na inakadiriwa kugharimu serikali asilimia 2.6 ya pato la Taifa kila mwaka.

Upotevu huu unatajwa kuwepo kwenye sekta ya Kilimo na husababishwa na ukuaji duni wa akili na mwili unaotokana na Utapiamlo.

Kutokana na hali hiyo Taasisi ya Chakula na Lishe nchini Tanzania(TFNC),shughuli za lishe zilianzishwa na Wizara ya Afya mnamo miaka ya 1950 kutokana na ripoti zilizoonyesha ongezeko la ukubwa wa vifo.

Makundi ya vyakula; Chakula Lishe.

Pia sababu nyingine ni ongezeko la magonjwa mbalimbali, tukio la njaa na uwepo wa vichocheo vingine ambavyo vilichangia ukuaji wa udumavu. 

Wahanga wakubwa wa tatizo hilo nchini watajwa kuwa ni wale watoto wa umri chini ya Miaka Mitano ambapo mtoto anapokoswa lishe bora huathirika Kiakili na hapo baadaye anaweza asifanye vizuri hata katika Elimu.

Kwa Mujibu wa Watalaamu hao wa Lishe ni kwamba Mtoto anapotimiza Umri wa Miezi 6 apewe vyakula vya nyongeza ili kukidhi mahitaji yake ya kilishe yanayoongezeka kadri anavyokua kwa kuwa maziwa ya mama pekeee hayawezi kutoshereza mahitaji ya kilishe ya mtoto.

Vyakula vya nyongeza anavyopaswa kupatiwa mtoto katika umri huo mbali na maziwa ya mama ni Vyakula vya nafaka,mizizi na vyakula vingine vyenye virutubisho,karanga au mafuta na maji safi na salama ya Kunywa.

Aidha,Vyakula vilivyo andaliwa kwa kutumia chumvi yenye madini joto  na kwamba Jitihada kubwa zilichukuliwa katika kupambana na kila hali kama vile kuzorota kwa hali kubwa ya afya katika idadi ya kundi la aina fulani la watu hasa kundi la watoto. 

Zaidi ya hayo mfumo wa ushirikiano wa sekta-mtambuka ilitumika na kupelekea maendeleo ya kuundwa kwa Kamati ya Ushauri ya Sekta-Mtambuka lengo lake kuu lilikuwa ni kutoa ushauri katika masuala mbalimbali ya lishe.

Kwa Mkoa wa Geita hali Lishe si ya kuridhisha kutokana na kuwepo kwa asilimia 38.9 ya Tatizo la udumavu licha ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula cha kutosha  nchini.


Mkuu wa wilaya ya Geita Willson Shomo.

Hali hii imeifanya serikali mkoani hapa kuwasainisha mkataba wa Lishe wakurugenzi wa Halmshauri zake ikiwa ni hatua ya serikali kukabiliana na tatizo la udumavu nchini.

Kwa Mujibu wa Afisa Lishe Mkoa wa Geita Riziki Mbilinyi anasema,kiwango hicho cha Udumavu ni sawa na takribani ya watoto laki moja wanakabiliwa na Udumavu.

Anasema,Tathimni ya sita ya kitaifa ya mkataba wa lishe ya mwezi Septemba 30, 2022, inaonyesha Geita imeshika nafasi ya pili kutoka mwisho. 

Akizungumzia tatizo la Utapiamlo katika Mkoa wa Geita Mbilinyi kwenye Utiaji wa Mkataba wa Lishe anasema kwa mwaka jana 2021/2022 takribani halmashauri nne za mkoa wa Geita hazikupanga bajeti kwa ajili ya watoto chini ya miaka mitano, ambayo ni Sh 1,000 kwa kila mtoto.

Halmashauri hizo vilevile hata kwenye matumizi halmashauri nne hizo hizo zimejikuta kwamba hazijatumia Sh 1,000 kwa kila mtoto.

Baba Mzazi akimpatia Mwanae Uji

“Ukiangalia kwenye matumizi ya fedha halmashauri ambayo angalau ilifanya vizuri ni halmashauri ya mji wa Geita na halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale.

“Halmashauri nne zilizobaki hazikufanya vizuri, yaani hazikutumia Sh 1,000 kwa mtoto, zilitumia chini ya Sh 1,000 na halmashauri hizo ni Bukombe, Chato, Mbogwe na Halmashauri ya wilaya ya Geita,” anasema.

Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita idara ya lishe inaendelea kuangalia viashiria vya tatizo la lishe na kupima kila robo ya mwaka katika ngazi ya halmashauri na mkoa kupitia vikao vya tathimini.

“Kigezo kilichotufanya tukashindwa kufikia malengo ni kigezo cha fedha, kwa sababu ukiangalia vigezo vyote tumefanikiwa kwa asilimia 80 lakini kwenye kigezo cha fedha tumefanikiwa kwa asilimia 50 tu,” anasema Mbilinyi.

Mikakati ya Kuimarisha Lishe mkoani Geita

Ili kuimarisha lishe ndani ya mkoa Riziki anasema “Tutahakikisha tunapeleka elimu kwa wananchi, kupitia kamati za chini kwa maana ya kamati ya maendeleo ya kata na kamati za huduma za jamii,” anasema.

Anasema kupitia kamati ya huduma ya jamii watahakikisha fedha ikiyotengwa kwa idadi ya watoto inawafikia walengwa kwa maana ya kuhudumia kundi la watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Riziki anaeleza, pia wamejipanga kusimamia suala la mlo kamili ngazi ya kaya, liweze kuzingatiwa ili kuondokana na tatizo la udumavu na kusababisha kushuka kwa afya na utapiamulo wa watoto.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita wa Geita, Martin Shigela ameelekeza wakurugenzi wa halmashauri kuchukua hatua stahiki kumaliza tatizo la udumavu wa watoto kwenye maeneo yao.

Shigela anasisitiza suala la bajeti ya halmashauri kwa ajili ya lishe ni suala la lazima na siyo ombi na kwa kufanya hivo utekelezaji wa sera na mipango ya kuimarisha lishe ndani ya mkoa itaweza kufanikiwa.

Aidha,amewataka maofisa lishe kutimiza wajibu wao kuwafikia wananchi kuwapatia lishe na kuondoa zana potofu na malezi duni yanayochangia watoto kukua katika mazingira hatarishi.

Nafasi ya Uzazi wa Mpango katika kuimarisha lishe

Akizungumuza baada ya kikao cha mapitio ya mkataba wa lishe halmashauri ya mji, Mkuu wa Wilaya Geita, Wilson Shimo anawashauri wananchi wilayani humo kuzaa idadi ya watoto wanaomudu.

Shimo anasema suala la lishe litafanikiwa ngazi ya familia iwapo wazazi watakuwa na idadi ya watoto wanaoweza kuwahudumia mahitaji muhimu ambayo ni malazi, mavazi na chakula.

Anasema serikali inafanya kazi kubwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo elimu na kwamba maendeleo ya elimu yatafikiwa iwapo wazazi nao watatimiza wajibu wao kwa watoto. 

“Rai yangu kwa watanzania na wana Geita wenzangu, tuendelee kuwa na mpango ambao utasaidia kuwa na watoto tunaoweza kuwasomesha, tunaweza kuwatunza, tunaweza kugharamia matibabu yao,” anasema Shimo.


Watoto wa darasa la Awali wakijisomea ikiwa moja ya sehemu ya Madarasa ya Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi,Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM).

Aliongeza pia kuwa na idadi ya watoto unaowamudu itawezesha kuimarisha ulinzi na maadili kwa watoto na kupunguza ama kuondoa tatizo la watoto kuishi katika malezi hatarishi kwa tabia na afya zao.

Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe Halmashauri ya Mji wa Geita, Dk. Konkamukula Clemence

 

Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe halmashauri ya mji wa Geita, Dk. Konkamukula Clemence anasema mafanikio ya suala la lishe ataenda sambamba na uzazi wa mpango.

Anasema ajenda ya masuala ya lishe ni lazima iambatanishwe na uzazi wa mpango kufanikisha mabadiliko ya lishe ndani ya jamii na kuondokana na tatizo la udumavu wa watoto.

“Uzazi wa mpango si idadi ya watoto pekee bali ni namna ya kupitanisha watoto kutoka mmoja hadi mwingine, huyu akue alelewe vizuri, afikie pahala fulani, ndio apatikane mwingine kwa wakati muafaka,” anasema Dk. Clemence. 

Anasema hayo yote ni kutokana na ukweli kwamba idadi ndogo ya watoto ndani ya familia inamupa nafasi mzazi ama mlezi kuweza kuwalea watoto na kuwapatia mulo kamili kadri ya mahitaji.

Dk. Clemence anasema uwepo wa vituo vingi vya kutolea huduma ndani ya halmashauri imewezesha ajenda ya uzazi wa mpango kuanza kueleweka ndani ya jamii na sasa mwitikio unazidi kukua.

Anakiri iwapo jamii itaendelea kuongeza mwitikio wa kuzaa kwa mpango ni wazi kwamba hata suala la lishe kuanzia ngazi ya kaya, halamshauri na hata mkoa litaweza kuimarika kadri ya malengo.

Afisa Lishe Halmashauri ya Mji wa Geita, Timotheo Mwendi anasema tathimini inaonyesha tatizo la udumavu wa watoto ndani ya halmashauri limepunguampaka kufikia asilimia 0.1 pekee.

Anakiri matumizi ya uzazi wa mpango yana nafasi kubwa kuimarisha lishe na utimamu wa afya ya mama na mtoto kwani bado kina mama wanakutana na changamoto za kiafya kutokana na kuzaaa mfululizo.

Anasema mama akiweza kuzaa kwa mpango inamusaidia kupata nafasi ya kuimarisha afya yake a kumtunza mtoto aliyenaye kabla ya kujifungua mtoto mwingine.

Wazazi Wanasemaje

Baadhi ya wazazi waliozungumza na Mwandishi wa Makala haya anasema kila mzazi akiwajibika kwa nafasi yake tatizo la Udumavu litapungua kwa kiasi kikubwa.

Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa Jina la Pendo John Mkazi wa Bombamili mama wa watoto wawili Mtoto akipata Lishe bora itasaidia kuwa na Afya njema na kuwa uwezo mzuri wa Kufikiri.


Wazazi wakimsikiliza Muunguzi mara baada ya kuhudhuria Kliniki ni kuhusu namna ya Kuwahudumia Lishe watoto kukabiliana na Udumavu.

Aidha,mzazi huyo anasema Changamoto inayoikabili jamii ni gharama kubwa za chakula jambo ambalo anaona kwake kuwa inaweza kuwa sehemu inayochangia kuwepo kwa Udumavu kwa watoto.

Anaongeza kuwa,uwepo wa watoto wengi kwenye familia kinatajwa kuwa chanzo kikubwa cha kupata mulo duni na lishe bora kwani kadri watoto wanavyoongezeka ndio gharama za kuwahudumia zinaongezeka.

Naye Oscar Samweli Mkazi wa Kijiji cha Bugulula anakiri kwamba, huduma ya chakula chenye lishe ndani ya familia kubwa ni tatizo na uhakika kipindi watoto wakiwa wachache ikilinganishwa na watoto wanapokuwa wengi ambapo gharama za chakula zinaongezeka.

Naye Gradiass John mama wa watoto watatu anasema ukiwa na watoto wachache kwa maana ya wawili ama watatu kama mzazi utamudu angalau kuwachukulia watoto matunda kila siku utokapo kazini,lakini ukiwa na wengi unashindwa kuangalia bajeti ya kesho yake.

Anasema wakati mwingine kina wazazi wanazidiwa na mahitaji ya watoto na wao kushidnwa kutoa huduma bora ya chakula kwa watoto na hivo kuishia kuwekeza kwenye uwingi wa chakula na siyo ubora.

Gradias anasema kuwa,ni kweli kama vijana wanaoanza maisha watahamasika kutumia uzazi wa mpango wana nafasi kubwa ya kuwalea watoto wanaowazaa kwa kuwatimia mahitaji kamili ya chakula na malazi. 

Hatua hii inakuja wakati tayari serikali ikiwa imezindua Programu ya Taifa ya Makuzi,Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM)unaolenga kumlinda mtoto kwenye masuala ya Elimu ya Awali,Lishe,Ulinzi na Usalama na Afya.

Programu hii iliyozinduliwa Disemba 14,mwaka jana wa 2021 inaenda sambamba na kuhakikisha kundi la watoto kuanzia mwaka 0 – 8 ambalo linahitaji kuangaliwa kwa karibu na kufanyiwa uwekezaji ili waweze kuwa rasilimali bora yenye tija kwa Familia na Taifa.

Katika Progaramu hiyo uwekezaji unaopaswa kufanyika ni pamoja na kukabiliana na tatizo la Udumavu,kuwapa huduma bora za malezi ya awali na program za elimu ambazo zitawawezesha kukua na kufikia ukuaji timilifu na hatimaye kuwa na watu wazima wenye uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji mali kwa Tija.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments