TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

FAHAMU KUWA;MTOTO HAWEZI KUFANISI DARASANI AKIWA ANAKABILIWA NA NJAA.

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga 

Na Salum Maige,Geita.

Ni vigumu kwa binadamu yeyote kufanya kazi au shughuli yoyote kwa ufanisi akiwa na njaa au akiwa dhaifu katika mwili wake kwa kwa sababu ya kukosa chakula au lishe.

Kwa wanafunzi inawawia vigumu kufikiria kikamilifu darasani akiwa na njaa kwa kukosa chakula anapokuwa shuleni.

Picha ya Wanafunzi wakipata chakula shuleni 

Ujifunzaji kwa mwanafunzi yoyote ni lazima uambatane na upatikanaji wa chakula ili aweze kujifunza vyema na kwa ukamilifu.

Ukosefu wa chakula shuleni huenda ukawaathiri zaidi wanafunzi hasa walioko darasa la awali  na la kwanza ambao umri wao ni mdogo zaidi  kuanzia miaka mine hadi saba ambao huhitaji kupata chakula kila wakati ukilinganisha na wale wenye umri mkubwa.

Kwa kuona hilo serikali imeagiza shule zote za msingi na sekondari kuanza kutoa huduma ya chakula kwa watoto ikiwa ni hatua ya kuboresha kiwango cha taaluma baada ya kugundua watoto wanafanya vibaya katika matokeo ya mtihani.

Inaelezwa kwamba,mwanafunzi hawezi kuzingatia na kuelewa kile anachofundishwa na mwalimu wake darasani kama atakuwa anakabiliwa na tatizo la njaa.

“a,a,e,e,i,i,o,o,u,u”, ni sauti za wanafunzi wa darasa la awali katika shule ya msingi Kukuluma Halmashauri ya mji wa Geita wakati wakiwa darasani wakifundishwa na mwalimu wao.

Sauti hiyo inanivutia masikioni mwangu wakati huo nikisogelea vyumba vya madarasa katika shule hiyo,napokelewa kwa tabasamu na mwalimu wa darasa ambaye alisogea mlangoni na kusalimiana naye.

Wakati tunazungumza mawili matatu na mwalimu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Elizabert John ambaye pia ni mwalimu mkuu wa shule hiyo nilishuhudia mmoja wa watoto akiwa amesinzia darasani humo.

Nilipouliza mwalimu alinijibu "Inaweza kuwa ni njaa au usingizi kwa sababu hawa watoto unakuta nyumbani wanalala muda umeenda au analala bila kula na asubuhi anaamshwa na mzazi wake kuja shule, na wakati mwingine njaa inaweza kumsumbua mtoto”.

Akizungumzia hali hiyo mwalimu anasema kuwa ,wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza huwa wanatoroka kwenda nyumbani na wanapouliza hudai wanaenda nyumbani kunywa chai.

Shule hiyo imeandikisha wanafunzi 51 wa darasa la awali na la kwanza wako 112, lakini kutokana na mwitikio mdogo wa wazazi kuchangia chakula wengi wao hutoroka darasani na kwenda nyumbani kutafuta chakula kutokana na njaa.

Ukiingia darasani unaweza kukuta watoto wengi hata 50 lakini ukitoka kidogo tu unakuta watoto wamepungua wamebaki hata 30 wakati mwingine 25,ukifuatilia unaona watoto wanaenda nyumba bila kutawanyishwa na sababu inayowafanya kutoka ni njaa”anasimlia Elizabert.

Anasema, wanafunzi wanaoongoza kutoroka wakati wa masomo ni wale wa darasa la awali na la kwanza na ambao ukiwauliza mara nyingi hudai wanakabiliwa na njaa.

“Inatuwia vigumu sana kuwathibiti hawa watoto,ukiwa unawarudisha wanalia wanasema njaa wanaenda kunywa chai nyumbani”anasema mwalimu huyo. 

Akizungumzia kuhusu maelekezo ya serikali ya kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi,mwalimu anasema, huduma ya chakula hutolewa lakini baadhi ya watoto hawapati chakula kutokana na wazazi kutochangia huduma hiyo.

Tulikaa kikao na wazazi tukakubaliana kila mwanafunzi atachangia shilingi 300 kila siku kwa ajili ya chakula ambapo fedha hiyo itakuwa inatolewa kila wiki shilingi 1,500, mtoto anapata chai kikombe kimoja na madazi mawili na siku zingine vipande vya viazi au mhogo na chai”, anasema mwalimu.

Licha ya makubaliano hayo na wazazi kuchangia huduma hiyo wanafunzi wanaopata chakula kutokana na wazazi wao kuchangia huduma ya chakula ni watoto wasiozidi 30, na mbaya zaidi wazazi wa wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza wengi wao hawachangii huduma hiyo.

Tunasikitishwa na mwitikio huu mdogo wa wazazi kuchangia chakula,lakini wakumbuke wazazi kuwa chakula hicho ni faida ya watoto wao,mtoto kumfundisha akiwa na njaa haelewi kabisa na unakuta kama hivyo anasinzia darasani au anatoroka”anasema mwalimu Elizabert.

Mwanafunzi Elias Pita wa darasa la kwanza anafurahishwa na huduma ya chakula kwani awali kabla ya huduma hiyo alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wanaondoka shuleni kabla ya muda na kwenda kusaka chakula nyumbani.

Mwanafunzi huyo alisikika akiwaambia wanafunzi wenzake akiwa darasani kwamba waandike vizuri na haraka ili kuwahi muda wa kwenda kupata chakula kitu ambacho kinamfanya mtoto huyo kufurahia huduma hiyo.

Baba alitoa hela sasa hivi siendi kunywa chai nyumbani nakula hapa nasoma baadaye tunaenda nyumbani sasa”anaongea na kuondoka huku akielekea eneo la huduma ya chakula.

Katika Kijiji cha Mwangimagi kata ya Nyanguku Halmashauri ya mji wa Geita viongozi wanafanya mkutano wa hadhara kuhamasisha wananchi kuchangia chakula shuleni lengo ni kuhakikisha maelekezo ya serikali yanatekelezwa.

Katika mkutano huo kaimu afisa elimu wa kata hiyo Emmanuel Ntungi ambaye pia ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nyanguku anasema,katika utafiti wa serikali umebaini wanafunzi kukosa chakula shuleni kunasababisha utoro na wanafunzi kutofanya vizuri.

tumewaiteni hapa ndugu zangu wananchi wazazi na walezi tuchangie chakula na kama inashindikana kabisa walau tutoe hata uji kwa watoto wetu shuleni wapate kula wakiwa shuleni”anasema Ntungi.

Awali katika mkutano huo afisa mtendaji wa kata hiyo Mnegela Tegezya amewaeleza wazazi kuwa, wasipuuze maelekezo ya serikali kwani hatua hiyo ni faida kwa watoto wao.

Jiulize hata wewe baba,mama unapochelewa kupata chakula,mfano umekuja kwenye mkutano kama huu tukachelewa kumaliza unaanza kulalamika njaa,je kwa mtoto mdogo ambaye anaamka saa 12 asubuhi na kwenda shule na kurudi saa 9 hadi saa 10 jioni bila kula wala kunywa maji inakuweje”anasema Tegezya.

Jumanne John mkazi wa kijiji cha Mwangimagi anasema, mwitikio mdogo wa kuchangia chakula unatokana na baadhi ya wazazi kushindwa kutambua umuhimu wa huduma hiyo kwa watoto.

Kwa sababu ni mwanzo ,tunaomba tu walimu na viongozi wa serikali waendelee kuwaelimisha wananchi kutambua umuhimu wa kuchangia chakula kwani hatua hiyo ni faida kwa watoto wetu,chakula ninachochangwa anakula mwanangu sasa shida nini”anasema Mariam Burashi.

Mkaguzi msaidizi wa polisi kata ya Nyanguku,Denis Simba Stephano,akiwa kwenye mkutano wa kamati ya ulinzi na usalama uliofanyika mtaa wa Kakonda mjini Geita amewaelekeza wazazi kuchangia chakula kwani kutofanya hivyo ni kutenda ukatili.

Amewaeleza wazazi kuwa,mzazi anayepuuza agizo na maelekezo ya serikali anakuwa ametenda kosa kwa sababu serikali ikishatoa maelekezo ni sheria.

Nawapongeza sana hapa Kakonda naona tayari wanafunzi wameshaanza kupata uji,lakini baadhi ya wazazi bado hawajataka kuchangia,kutofanya hivyo ni kosa na kwamba mtoto kumnyima chakula ni kumfanyia ukatili mkubwa,hivyo nawaomba sana wananchi tujitoe kuchangia huduma hii muhimu”anasema Stephano.

Mkaguzi msaidizi wa Polisi kata ya Nyanguku Denice Simba Stephano akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Mwangimagi baada ya kikao cha kuhamasisha utoaji wa huduma ya chakula shuleni. 

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kakonda Joseph Mshipi anasema, wazazi katika Mtaa huo wameitikia kuchangia huduma ya chakula lakini baadhi ya wazazi bado wanasuasua na jitihada za kuwahamasisha zinaendelea.

Afisa elimu mkoa wa Geita Anton Mtweve anasema,serikali mkoani huo imeshazielekeza shule zote kuanza kutoa huduma ya chakula na wazazi wanapaswa kuwajibika juu la huduma hiyo.

Mtweve amesema, kwa kuanzia serikali imezielekeza shule zenye mashamba kuanza kulima mazao ya shule kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi.

Tumeona kwamba kutokana na hali ya chakula kuwa ngumu,tumeelekeza wazazi na walezi walau waanze kuchangia kwa kutoa hata uji kwa wanafunzi,hii itasaidia kuwangika na njaa kabla ya kufika muda wa kwenda nyumbani”anasema Mtweve.

Mkoa wa Geita una jumla ya shule za msingi 763 kati yake za serikali ni shule 693 na kwamba kwa mwaka huu zimeweza kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza na awali 189,966 kati yake wanafunzi wa awali 75,056 na la kwanza 114,910.T

Aidha,oktoba 29,2021 wizara ya elimu sayansi na teknolojia ilizindua mwongozo wa kitaifa wa utoaji huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu msingi.

Mwongozo huo unalenga kujenga uelewa wa pamoja wa wadau wa elimu na jamii ili kutekeleza kikamilifu mpango huo kwa wanafunzi.

Hivi karibuni,naibu waziri wa elimu sayansi na teknolojia Mhe.Omary Kipanga amesema, utoaji wa chakula na lishe kwa wanafunzi wakiwa shuleni ni suala muhimu kwa kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya afya ya mwanafunzi na maendeleo yake kitaaluma.

Anasema,mwanafunzi anapokosa chakula shuleni hukosa usikivu wakati wa ujifunzaji,mahudhurio hafifu,utoro wa rejareja na hata wakati mwingine hukatisha masomo baada ya kutoroka kutokana na njaa.

Pamoja na jitihada za serikali kutaka kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji,upatikanaji wa matokeo mazuri ya elimu hutegemea afya aliyonayo mwanafunzi,afya ambao inatokana na chakula na lishe.

Mtaalamu wa elimu ya awali kutoka shirika la Children in Crossfire(CiC) nchini Tanzania Davis Kisuka anasema,moja ya vitu vya lazima katika ukuaji wa ubongo wa mtoto ni chakula.

Anasema,mtoto anapopata chakula na kushiba ubongo wake hukua kwa kazi katika kufikiri na kufanya maamzi,lakini inapotokea mtoto anakuwa na njaa hukabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo hivyo ubongo wake unadumaa.

Njaa hufanya mtoto kuwa mnyonge sana,lakini anapokuwa ameshiba hata humsaidia kushiriki michezo mbalimbali  na watoto wenzake,hivyo wazazi wanatakiwa kuunga mkono juhudi hizi za serikali za kutoa chakula kwa wanafunzi” anasema Kisuka.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 27 barani Afrika iliyotia saini fomu ya kujiunga na Muungano wa nchi zinazotoa chakula shuleni ikiwa ni kumwezesha mwanafunzi kupata lishe  bora,Afya na elimu.

Nchi zingine zilizotia saini makubaliano hayo ni Angola,Benin,Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Chadi, Jamhuri ya Kimekrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Gambia,Guinea,Kenya,Lesotho,Liberia,Madagasca,Mali,Maurtania,Morocco,Msumbiji,Namibia,Niger,Jamhuri ya Kongo, Rwanda,Senegal,Somalia na Sudan.

Mkurugenzi mkazi wa shirika la umoja wa mataifa la mpango wa chakula Duniani(WFP)Sarah Gordon Gibson anasema,hatua ya nchi hizo kuanza kutoa huduma ya chakula kwa watoto itakuza uelewa na kuchocheza ukuaji wa ubongo wa mtoto.

Ameongeza kuwa,utafti unaonyesha kuwa njaa ni moja ya kikwazo kikubwa kwa mtoto kuelewa pale anapokuwa anafundishwa kwani ubongo wake hushindwa kufanya kazi vizuri ambapo badala ya kuelekeza fikira zake kujifunza anafikiria shida ya njaa aliyonayo.

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments