Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) CPA Beng'I Issa |
Na Urban Epimark, KIGOMA.
Maonesho ya Sita ya Mifuko ya Program za Uwezeshaji hapa nchini yanayo ratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) yanayo endelea katika mji wa Kigoma katika viwanja vya Mwanga Community Centre yamekuwa ya manufaa makubwa kwa wakazi wa Kigoma wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara.
Maonesho hayo yaliyo anza Mei 21, 2023 yanatarajiwa kufikia tamati siku ya Jumamosi Mei 27, 2023 na Mgeni Rasmi siku hiyo ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa, huku yakiongozwa na Kaulimbiu "kutumia mabadiliko ya kidigitali katika mifuko ya uwezeshaji pamoja na program zake"
Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ushiriki wa Watanzania kutoka Ofisi ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Makao makuu Dodoma, Bi Neema Mwakatobe amewaeleza waandishi wa habari kwenye maonesho hayo kwamba, idadi kubwa ya wakazi wa mkoa wa Kigoma na mikoa ya jirani wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara zaidi ya sabini (70) wamefanikiwa kupatiwa mafunzo ya Uwezeshaji kutoka kwa taasisi mbalimnali zilizo andaliwa kufundisha madarasa ya wajasiriamali kwenye maonesho hayo.
Lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa umma wa mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa ya jirani kupata elimu mbalimbali kutoka kwa taasisi zinazo jishughulisha na urasmishaji biashara za wananchi ili kuwapatia elimu ya jinsi ya kunufaika na program za mifuko mbalimbali ambayo ni sabini na mbili (72) iliyopo chini ya uratibu wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili wananchi waijue na kuitumia kuendeleza biashara zao na kusaidia kutoa ajira na kuondoa umaskini nchini.
Mbali na madarasa ya mafunzo kwenye maonesho hayo ambapo palitengwa wasaa wa kutosha kwa taasisi mbalimbali kutoa mafunzo, NEEC iliandaa pia meza maalum kwa kila taasisi kwenye maeneo ya viwanja vya maonesho kukutana na wanao fika kwenye hayo maonesho ili kupatiwa ufafanuzi wa mambo kadhaa wa kadhaa.
Kwenye banda la NEEC, Afisa Uwezeshaji Mwandamizi anae shughulikia masuala ya ushiriki wa watanzania kwenye miradi ya kimkakati (Local Contents) Bi Sizan Massala alitoa maelezo ya ufafanuzi kwa watu wa kada mbalimbali waliofika kwenye meza ya NEEC kuhusu Baraza linavyo wezesha kampuni za kitanzania kukua kiuzalishaji na pia kuwa na vigezo vya kutoa huduma na uuzaji wa bidhaa kwenye miradi mikubwa inayo jengwa nchini pamoja na maeneo ya wawekezaji kutoka nje ya Tanzania.
Moja ya Mafanikio makubwa ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi anaeleza Afisa Uwezeshaji wa NEEC Bw Omar Haji kutoka Kitengo cha Uratibu wa Mifuko na program za uwezeshaji kwamba ni kuanzishwa kwa mpango wa uchumi wa viwanda unaoitwa SANVN VIWANDA SCHEME.
Mpango huu unatoa mikopo kwa wenye viwanda wajasiriamali wadogo kuanzia milioni 8 hadi milioni 50, wajasiriamali wa kati ni milioni 50 hadi milioni 500.
"Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) linajivunia kuanzishwa kwa mpango wa SANVN VIWANDA SCHEME kwa kushirikiana na taasisi tano za NEEC, SIDO, VETA, NSSF na Benki ya Azania" anaeleza Afisa Uwezeshaji Bw Omar Haji.
Bw Haji anaendelea kuelezea mafanikio katika mpango wa viwanda scheme ya kwamba, kampuni za kitanzania nyingi zimeanzishwa na kuwezesha kutoa ajira nyingi pamoja na kuchangia patoa serikalini na kupunguza umaskini kupitia Baraza la Uwezeshaji kwa kuwezeshwa mikopo ya uwekezaji (investment loans) na mikopo ya uendeshaji kampuni hizo yaani working capitals.
Mifano halisi ya wanufaika wa mpango wa SANVN VIWANDA SCHEME ni kampuni ya B & L Agri-Digital ya jijini Dar es Salaam iliyo wezeshwa mtaji wa kujiendesha (working capital) ambapo kampuni hiyo kwa sasa ina zalisha mafuta ya Alizeti ya chapa au brand ya San Rich yenye ubora wa kimataifa (triple refinary edible oil) na kuyafungasha kwenye vifungashio sahihi vyenye kuhimili ushindani sokoni lakini pia katika ujazo wa hali zote (mdogo, kati na mkubwa) na kuwezesha mwenye kipato kidogo na kikubwa kununua.
Kampuni hiyo iliyo anzishwa nchini mwaka 2019 ambayo ilianza kwa kufanya utafiti kuhusu changamoto za upatikanaji mafuta ya kupikia, imewezesha kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania jijini Dar es Salaam na Dodoma zaidi ya 50 na pia inachangia pato serikalini kwa kulipa kodi na kwa sasa inauza bidhaa zake nyingi katika mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara, Songea lakini pia Morogoro, Pwani na Kahama.
Meneja wa Mauzo wa B & L Agri-Digital Bw Frank Kilongola anaeleza zaidi kwamba, kampuni hiyo inalenga miaka ya usoni kuuza bidhaa zake nje ya nchi hususani kwenye maduka makubwa (Supermarkets) kwani wanavyo vigezo vyote vya kuuza nje ya mipaka ya Tanzania ikiwemo Barcodes kutoka GS1-Tanzania.
Mnufaika mwingine wa mpango wa SANVN VIWANDA SCHEME ni kampuni iliyoanzishwa na kuongozwa na mwanamama wa kitanzania Bi Violet Oscar pia kutoka mkoani Dar EsSalaam anae miliki kampuni ya kutengeneza vijiti vya meno (toothpicks) na vibaniko vya nyama (bamboo skewers)
Watanzania wengi wanakumbuka jinsi wabunge wetu walivyo kuwa siku za nyuma wakilalamikia uagizaji wa vijiti vya meno, sindano na hata nyembe kutoka nje, ambapo kampuni za kitanzania hazikuwa kutengeneza bidhaa hizi nchini.
Lakini kwa kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) chini ya mpango wa SANVN VIWANDA SCHEME mtanzania huyu mwanamke amewezeshwa mtaji na sasa ameondoa pengo la Tanzania kuagiza vijiti vya meno kutoka China.
"Nina shukuru Baraza la Uwezeshaji (NEEC) kunishika mkono kuniwezesha hadi nimeanzisha na kumiliki kampuni yangu ya Bongo Toothpicks Industry na sasa nimeweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya hamsini (50) na pia kulipa kodi serikalini na pia kuwezesha bidhii hizi kupatikana nchini" anaeleza Bi Violet Oscar Mkurugenzi wa Bongo Toothpicks Industry. |
Bi Violet Oscar anaeleza historia yake kwamba alikuwa mwajiriwa katika taasisi fulani hapa nchini. Hakuridhika na maisha ya kuajiriwa. Kipindi hicho ndipo Tanzania ilikuwa ikihimiza sera ya Tanzania ya Viwanda na ndipo yeye akaiona fursa ya kutengeneza vijiti vya meno na kujifunza ujuzi wa kuvitengeneza kwa njia ya kusoma mtandaoni. Huu ni ujasiri mkubwa sana kwa mwanamke wa kitanzania.
Alimpata mtaalam kutoka nchini China ambae walikuwa wakiwasiliana kwa mtandao lakini bila wao kujuana uso kwa uso. Raia huyu wa China alimfundisha na kumwelekeza kwa njia ya mtandao na pia kumtumia aina ya mashine ya kutengeza bidhaa hiyo.
Bi Violet Oscar kipindi hicho alikuwa akizalisha kwa kutumia mianzi ya kienyeji (Local bamboo trees) na eneo lake la uzalishaji lilikuwa Bunju, Dar es Salaam.
Aliamu kujiendeleza kwa kupata mafunzo zaidi SIDO na baadae kuomba mkopo kupitia SANVN VIWANDA SCHEME na kuwezeshwa mtaji wa kupanua uzalishaji wake. Alipewa mkopo wa kununua mashine na vipuli vya kutosha na kuhamishia kiwanda chake wilayani Kisarawe mkoani Pwani na kwa sasa ameajiri watanzania zaidi ya hamsini (50) na analipa kodi serikalini, huku akisema anaona mafanikio makubwa siku za usoni kibiashara.
Changamoto anazo kutana nazo Bi Violet Oscar katika uzalishaji wake lakini pia kwa upande wa pili ni fursa kubwa kwa wakulima, ni uhaba wa miti ya kisasa ya mianzi kwa ajili ya kuzalishia vijiti vya meno na vibaniko vya nyama.
"Nimeshaenda kuonana na Wakala wa usimamizi na uendelezaji misitu hapa nchini yaani TFS na kuwaelezea changamoto yangu kuhusu ukosefu wa miti ya kisasa ya mianzi na wao wameshanielewa. TFS wamesha anzisha vitalu vya miti ya mianzi ya kisasa (hybrid bamboo trees) na kwa sasa wana karibia kuvuna" anaeleza Bi Violet Oscar.
Katika kuhitisha makala hii, zipo shuhuda nyingi kwa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa manufaa ya watu wa Kigoma kupitia maonesho haya ya Sita (06) ya mifuko ya uwezeshaji na program zake hapa nchini.
Wito umeendelea kutolewa kwenye maonesho hayo kwamba, wananchi wa mjini Kigoma na maeneo ya jirani waendelee kufika kutembelea maonesho hayo kwani bado muda upo, ili wajifunze kwa hawa wachache wenye shuhuda za mafanikio ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaani NEEC.
Mwisho.
0 Comments