TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

WAZAZI/WALEZI MJINI GEITA WAELIMISHWA KUTHIBITI WIMBI LA UKATILI KWA WATOTO

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu, Dkt Dorothy Gwajima.

Salum Maige,Geita.

Inaelezwa kuwa,hakuna faida inayoweza kupatikana kwa kutumia gharama kubwa kusomesha mtoto kama wazazi na walezi hawatahusika katika kusimamia suala la ulinzi na usalama wa mtoto dhidi ya matukio ya ukatili yakiwemo ya ubakaji na ulawiti.

Athari ya ukatili dhidi ya watoto inapelekea kuongezeka kwa idadi kubwa ya watoto wanaoacha shule,kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa na yasiyokuwa na tija kwenye jamii na taifa kwa ujumla.

Matukio hayo, mengi yametajwa kufanywa na watu wa karibu na familia ya mtoto wakiwemo ndugu,jamaa na majirani.

Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na matukio ya ukatili dhidi ya watoto hapa nchini yakiwemo mauaji,ubakaji na ulawiti hali inayotishia usalama wa mtoto ambapo hivi karibuni katika mtaa wa Mwatulole mtoto wa miaka mine anadaiwa kulawitiwa na wachungaji wawili wa mifugo.

Pia disemba mwaka jana katika mtaa huo wa Mwatulole kijana Jabir Hamis alikamatwa na wananchi na kumshambulia kwa kipigo baada ya kukutwa akiwa na watoto wadogo wakiwemo wa umri wa miaka mitano na minane akiwafundisha vitendo vya ushoga na ulawiti.

Matukio hayo yameishitua serikali mkoani hapa na hivyo kuanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya ulinzi na usalama kwa watoto wao ili kuwalinda dhidi ya matukio hayo ambayo huwaathiri katika makuzi yao.

Mkuu wa polisi dawati la jinsia,wanawake na watoto wilaya ya Geita mkaguzi msaidizi wa polisi Christina Katana amesema,jukumu la ulinzi wa mtoto ni la kila mmoja katika jamii ili kutokomeza ukatili huo.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Shinamwenda kata ya Nyanguku halmashauri ya mji wa Geita Katana amesema ,hakuna uwekezaji wenye faida kubwa katika jamii na taifa kwa ujumla kama ulinzi wa mtoto.

Mkuu wa dawati la jinsia,wanawake na watoto wilaya ya Geita Mkaguzi msaidizi wa polisi Christina Katana akizungumza na wananchi wa kijiji cha Shinamwendwa mjini Geita kwenye mkutano wa hadhara wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuwalinda watoto.

Hakuna faida inayoweza kupatikana kutumia gharama kusomesha mtoto halafu unashindwa kumlinda,sasa mtoto yuko chekechea ,darasa la kwanza na kuendelea unatumia gharama kusomesha halafu mtoto akikuwa anakuwa shoga utakuwa na faida gani?”aliuliza Katana.

Amesema kuwa, kuna watoto wana ndoto kubwa katika Taifa hili ,lakini ndoto hizo wanashindwa kuzifikia kwa sababu ya kukabiliwa na matukio ya ukatili yakiwemo ya kipigo,ubakaji na ulawiti matukio ambayo yamekuwa yakiwaathiri kisaikolojia.

Kuna suala la sisi wazazi pande zote mbili wanawake na wanaume tunawafanyia watoto ukatili kwa kumnyima haki zake za msingi na hasa za kimalezi ambapo watoto wanaachwa na kwenda kwenye maeneo yasiyofaa na huko ndiko wanabakwa na kulawitiwa”anasema Katana.

Katika ziara ya kiongozi huyo amekukutana na wanafunzi wa shule ya msingi Shinamwendwa na kuzungumza na watoto hao pamoja na mambo mengine kuwaelimisha juu ya kutoa taarifa zinazoashiria ukatili dhidi yao.

Simon Kasila mkazi wa kijiji cha Shinamwenda amesema,kuna baadhi ya maeneo ambayo yanatishia kuwepo kwa ukatili yakiwemo maeneo yenye mashine za michezo ya kubahatisha maarufu kwa jina la bonanza ambapo watoto wenye kuanzia umri wa miaka mine huonekana katika maeneo hayo.

Mkuu wa dawati la jinsia,wanawake na watoto wilaya ya Geita,mkaguzi msaidizi wa polisi Christina Katana akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Shinamwendwa halmashauri ya mji wa Geita juu ya kuwapa elimu ya kutoa taarifa za ukatili.

Tunaomba sana serikali inayotoa vibali vya michezo hiyo izingatie mazingira ya kuweka mashine hizo ambazo kawaida inatakiwa ziwe kwenye maeneo yasiyo ya wazi,hali hiyo ni hatari sana katika usalama wa mtoto”anasema Kasila.

Regina James mkazi wa Nyanguku amelipongeza jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia,wanawake na watoto kutoa elimu ya kuwalinda watoto dhidi ya matukio ya ukatili hatua itakayosaidia watoto kuishi salama.

“Tunampongeza sana huyu mama kuja kutuelimisha juu ya kuwalinda watoto wetu,kwani huku matukio ya watoto kufanyiwa ukatili wa kupigwa,kupewa adhabu zilizopitiliza na wazazi na walezi wao hutokea kila wakati”.anasema Regina.

Ameongeza kuwa,baadhi ya watoto wanafanyiwa ukatili wa kunyimwa haki yao ikiwemo ya kupata elimu kwa kupewa kazi za nyumbani ikiwa ni pamoja na kulea wadogo zao wakati wazazi wakiwa kwenye shughuli za kilimo na ufugaji.

Baadhi ya wazazi na walezi katika kijiji cha Shinamwendwa mjini Geita wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakimsikiliza mkuu wa dawati la jinsia,wanawake na watoto wilayaya Geita wakati akitoa elimu ya kukabiliana na matendo ya ukatili kwa watoto.

Aidha,katika kuunga mkono juhudi hizo za kukabiliana na ukatili kwa mtoto,mtendaji wa kata ya Nyanguku John Shatta amepiga marufuku michezo ya bonanza katika kata hiyo kutokana kuendeshwa kinyume na leseni.

Amefafanua kuwa,michezo hiyo inatakiwa kuwa kwenye maeneo ya starehe na hivyo mashine hizo hazitakiwi kuwa katika maeneo ya vijijini ambako hakuna maeneo ya kumbi za starehe.

Hata hivyo,katika taarifa ya programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto(PJT-MMMAM) ya mwaka 2021/22 hadi 2025/26 inasema kuwa,kuna upungufu mkubwa wa utoaji wa taarifa za vitendo vya unyanyasaji na utelekezaji wa watoto kuanzia miaka 0 hadi 8.

Taarifa hiyo inafafanua kuwa,katika utafiti mdogo uliofanywa kwenye jamii kuhusiana na kesi za ukatili,unyanyasaji na utelekezaji wa watoto wadogo unafanywa zaidi na wazazi na walezi.

Aidha,Takwimu za jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kuwa,katika kipindi cha januari hadi disemba ,2021 matukio 11,499 ya ukatili yalitolewa taarifa kwenye vituo vya polisi na mikoa iliyoongoza ni Arusha(808),Tanga(691),Shinyanga(505),Mwanza(500)na mkoa wa kipolisi wa Ilala(489).

Makosa yanayoongoza kwa idadi ni ubakaji(5,899),mimba kwa wanafunzi(1,677) na ulawiti(1,114).

Juni 6,mwaka jana akiwa mkoani Dodoma katika shule ya Msingi Mnadani alipokuwa akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule hiyo,Waziri wa Maendeleo ya Jamii,jinsia,wanawake na makundi maalumu, Dkt Dorothy Gwajima aliwataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya vitendo vya kikatili dhidi yao vinavyotokea maeneo ya nyumbani,shule na njiani.

Kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya Na.21 ya mwaka 2009 inasema kuwa,kila mtoto anayo haki ya kuishi na kupata malezi bora,ulinzi na kuendelezwa bila aina yoyote ya ubaguzi na kwamba mtoto mtoto anapokuwa nyumba au kwenye jamii anapaswa kulindwa dhidi ya ukatili na kuhakikisha usalama wake.

Ili kutomeza ukatili huo jamii inapaswa kushirikiana kikamilifu katika kutoa taarifa za matukio hayo na wazazi na walezi kuwa walinzi wa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwakagua sehemu za miili yao.

Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments