TANGAZA NASI: geitapressclub@gmail.com

ZAHANATI YA NYAMALEMBO; MAPINDUZI YA HUDUMA ZA AFYA KWA AKINA MAMA GEITA MJINI

Salum Maige, Geita 01/08/2024

Kukamilika kwa zahanati ya Mtaa wa Nyamalembo halmashauri ya mji wa Geita mkoani Geita kumesaidia kuwapunguzia wananchi hasa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kufuata huduma za afya.

Awali, wakazi hao walitegemea kupata huduma hizo kwenye hosptali ya halmashauri ya mji wa Geita, na kituo cha Afya Nyankumbu ambapo kufika huko walitumia zaidi ya masaa saba kwenda na kurudi nyumbani.

Aidha,moja ya sababu zinazotajwa kuchangia vifo vya wajawazito na watoto wachanga ni umbali wa kufikia huduma za Afya na ubovu wa miundombinu ya barabara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakiwa kwenye Zahanati hiyo baadhi ya akina mama wamesema, kusogezwa kwa huduma hiyo kumewasaidia kupata huduma za Afya karibu na wamekuwa wakitumia muda mfupi kurejea nyumbani.


“Zamani tulikuwa tunahangaika mno na ukiangalia mazingira ya huku kwetu ni milima na mabonde, tulilazimika kutumia usafiri wa pikipiki kwenda kituo cha afya Nyankumbu na mjini.Kwa mama mjamzito hasa nyakati za usiku ndo ilikuwa shida kubwa” anasema Neema Mussa.


Ameongeza kuwa, walikua wakifika wamechoka na wakati mwingine baadhi ya akina mama  walikua wakichelewa kuanza huduma ya kliniki ya ujauzito na kupelekea  baadhi ya watoto kukatisha huduma ya kliniki kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano. 

Kwa upande wake Elizabert Williamu mkazi wa mtaa wa Nyantorotoro "B" anasema kutoka nyumbani hadi kwenye zahanati hiyo anatumia takribani dakika 15 tofauti na kipindi cha nyuma ambapo alitumia dakika 40 kufikia huduma za afya.

“Tunaipongeza  serikali kwa kutujengea zahanati, mwanzoni hatukuwa na matumaini kwamba tutapata zahanati ,lakini viongozi wa mtaa ,kata na mbunge wetu wametusaidia kwa kiasi kikubwa , lakini pia waandishi wa habari wamesaidia kwa kiasi kikubwa  kuandika tatizo hilo hata viongozi wasingejua kama tunachangamoto ya kukosekana kwa zahanati"  alisema Elizabert.

Samson Daud baba wa familia ya mke na watoto wawili anasema, hapo mwanzo mtoto wake alizaliwa katika hospitali ya Geita lakini alihangaika sana kumfikisha huko kutokana na eneo hilo kuwa na milima na mabonde makubwa.

“Mke wangu alifika amechoka kweli,hivyo ujio wa huduma hii kwetu ni faraja kubwa sana mtoto wangu huyu wa pili amezaliwa hapo na hatukutumia muda mwingi kufika. Hivyo mimi niseme tu tunaipongeza sana serikali kutujali sisi wananchi wa Nyamalembo” anasema Daud.

Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Amoud Yahya anasema kwa siku zahanati hiyo inahudumia watu zaidi ya 400 kwa mwezi na kati yao wanaojifungua ni 10 hadi 15.

“Imesaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano,kwa mwezi tunaweza kupokea kesi moja ya mama kujifungulia nyumbani, hivyo uwepo wa zahanati hii katika eneo hilo imesaidia sana wananchi”, amesema Yahya.

Akizungumzia sekta ya Afya mbunge wa jimbo la Geita mjini Costantine Kanyasu amesema ,wakati anaingia madarakani mwaka 2015 jimbo lake ambalo linaunda halmashauri ya mji wa Geita lilikuwa na kituo kimoja cha afya cha Kasamwa lakini tumeongeza na kufikia vitatu, mbali na vituo hivyo vya afya zahanati nazo zimeongezeka ambapo karibu kila kijiji kina zahanati na baadhi ya mitaa ina huduma hiyo.

“Lengo langu ni kuhakikisha tunasogeza huduma kwa jamii kuwapunguzia wazazi kutembea umbali mrefu kwenda kujifungua na kliniki ya ujauzito na watoto chini ya miaka mitano, ambapo mama akikutwa na tatizo la uzazi pingamizi anapata huduma karibu ili kuokoa uhai  wa mama na mtoto aliyeko tumboni” anasema Kanyasu.

Aidha, serikali ya mkoa wa Geita inasema upungufu wa watalaamu wenye sifa,uhaba wa vifaa tiba vinavyoweza kutumika pindi watoto wachanga wanaposhindwa kupumua na ubovu wa barabara vimetajwa na mkoa kuwa ni sababu zilizochangia vifo vya watoto wachanga 337 kuanzia januari hadi mei mwaka huu 2024.

Kwa mujibu wa kaimu katibu tawala mkoa wa Geita, Herman Matemu alisema, hayo juni 24,2024 wakati akiwapokea madaktari bingwa 35 waliofika mkoani humo kutoa huduma za kitabibu kwenye hospitali sita za halmashauri sita za mkoa wa Geita kwa siku tano

Alisema, sababu hizo pia,zimechangia vifo vya uzazi kwa akina mama 24 kwa kipindi hicho na kuwataka watumishi wa sekta ya afya ambao hospitali zao zinafikiwa na madaktari  bingwa watumie fursa hiyo kujengewa uwezo, kujifunza mbinu mpya ili baadaye wawasaidie wananchi wenye matatizo ya kiafya.

Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt.Omar Sukari amesema mkoa huo wenye wakazi milioni 2.9 una vituo vya kutolea huduma 247 na kwa miaka mitatu iliyopita vituo vipya 63 vimefunguliwa na 27 kati ya hivyo vinatoa huduma ya upasuaji.

Dkt. Sukarii amesema, katika mkoa wa Geita akinamama 120,000 hujifungua kila mwaka.

Akitoa takwimu za miaka mitatu  nyuma, Dkt.Sukari amesema, kwa mwaka 2021 kina mama 63 walipoteza maisha ,mwaka 2022 akina mama 57 walipoteza maisha na mwaka jana 2023 akina mama 55 na mwaka huu wa 2024 kuanzia januari hadi mei akina mama 24 walipoteza maisha kabla,wakati na baada ya kujifungua.

Kwa upande wa watoto amesema, mwaka 2022 vifo vilikuwa 905,mwaka 2023 vifo 817 na mwaka huu  kuanzia januari hadi mei  2024 watoto wachanga 337 wamepoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kupumua na kuzaliwa na uzito pungufu usio wa kawaida.

Amesema vifo hivyo vimeendelea kupungua kutokana na serikali kuboresha huduma za afya kama vile ujenzi wa miundombinu, ujenzi wa zahanati hasa maeneo yaliyo mbali na vituo vya afya na ununuzi wa magari ya kubeba wagonjwa.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Afya la umoja wa mataifa(WHO) inasema Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2030 wanawake 390 watakufa wakati wa kujifungua kwa kila vizazi hai 100,000.

Hii ni zaidi ya mara tano zaidi ya lengo la ajenda ya mwaka 2030 la vifo vya chini ya 70 vya uzazi kwa kila vizazi hai 100 000, na iko juu sana kuliko wastani wa vifo 13 kwa kila watoto 100 000 wanaozaliwa hai iliyoshuhudiwa barani Ulaya mwaka 2017 na pia ni zaidi ya kiwango cha kimataifa cha wastani wa vifo 2011. 

Mwisho.

Muonekano wa zahanati ya Nyamalembo halmashauri ya mji wa Geita.


Mhudumu wa afya katika zahanati ya Nyamalembo akitoa huduma ya chanjo kwa watoto




Post a Comment

0 Comments