Matumizi ya nishati ya jua (solar) hasa kwenye kilimo cha umwagiliaji
kinatazamwa na wakulima wa mboga mboga wa kijiji cha Nyamgogwa wilayani
Nyang`hwale mkoani Geita kuwa, ni
suluhisho katika kukabiliana na gharama za uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na
mabadiliko ya tabia nchi.
Kijiji hicho kinakadiriwa kuwa na wakulima wa mboga mboga
zaidi ya 200 ambao hulima nyanya, kabechi, chainizi, mchicha na matikiti maji hutegemea
maji ya kumwagilia kutoka kwenye bwawa lililopo kando ya mashamba yao.
Pampu zinazotumia nishati ya jua (solar) sio tu inapunguza gharama za kilimo, bali inachangia
kuongeza uzalishaji wa mazao hasa kwenye maeneo yenye ukame na yenye changamoto
ya upatikanaji wa maji.
Teknolojia hiyo ni nafuu kutokana na kutohitaji fedha za
kila siku kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendeshea jenereta la kusukuma maji
kwenda kwenye mashamba kutoka kwenye vyanzo vya maji.
Katika kijiji cha Nyamgogwa wakulima wanasema, teknolojia
hiyo ikiwafikia itawasaidia kupunguza muda wanaotumia kwenye umwagiliaji
unaotumia mikono na gharama za mafuta ya kuendesha jenereta hasa kipindi cha kiangazi.
Teknolojia hiyo ya umwagiliaji kwa kutumia nishati ya jua (Solar) inatumiwa na afisa kilimo wa kata
ya Shabaka, Mlyomi Dunia ambaye amefunga mitambo hiyo kwenye shamba lake hali
iliyoleta shauku kubwa kwa wakulima wa
mboga mboga kijijini hapo.
Aidha, wakulima Hasani Shilole na Charles Misalaba ni miongoni mwa wakulima ambao mazao yao humwagilia kwa kutumia mikono na wakati mwingine hutumia jenereta kuvuta maji, wanasema kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya nishati ya jua(solar) ni rahisi ukilinganisha na umwagiliaji wanaotumia kwa wakati huu.
“Tunamwagilia kwa kutumia mikono kwa kuajiri vibarua kwa
siku ama kwa mwezi na tunawalipa
shilingi 100,000 hadi 200,000 kwa mwezi kutegemeana na ukubwa wa shamba,
pamoja na kufanya hivyo huwa hatujui soko letu litakuweje, hivyo unaweza
kutumia gharama kubwa halafu soko linakuwa sio zuri” anasema Hasani Shilole.
Shilole ameongeza kuwa, wakati mwingine huwalazimu kuamka
saa 11 alfajili kwenda kumwagilia akiwa yeye, familia yake na vibarua ambapo
hutumia zaidi ya saa nne hadi tano kumwagilia kwa mikono shamba lenye ukubwa wa
ekari moja.
Naye mkulima Hadija Francis anasema, endapo serikali na
taasisi zinazouza paneli za nishati ya jua watawakopesha wakulima, itawasaidia kuepuka gharama za uendeshaji wa jenereta pia
kupunguza muda wa kumwagilia na usumbufu.
“Tunatamani sana kulima kilimo cha kisasa cha mfumo wa
nishati ya jua(solar) kwani wakati wa kiangazi tunatumia muda mwingi sana na
maji hukauka hivyo, tunayatoa mbali na eneo tunalomwagilia ni dogo”, anasema Hadija.
Mkulima mwingine Mashaka Salu anayesjishughulisha na kilimo
cha nyanya anasema, teknolojia ya nishati jua inaweza kuwarahisishia maisha kwa
sababu umwagiliaji wa jenereta ni ghali sana ambao huwalazimu kila siku kuwa na
fedha ya kununua mafuta ambayo nayo hupanda bei kila wakati.
“Nimetembelea eneo linalotumia umwagiliaji wa mfumo wa nishati jua, nimevutiwa na mfumo huo, lakini tunashindwa kununua paneli hizo kwani zina gharama kubwa lakini ukishafunga umemaliza, hivyo naomba serikali itusaidie kuhusu teknolojia hiyo ya kisasa ikiwezekana itukopeshe tuwe tunalipa kidogo kidogo” anasema Mashaka Salu
Hata hivyo, kwa mujibu wa afisa kilimo kata ya Shabaka,
Mlyomi Dunia, anasema wananchi wa kijiji cha Nyamgogwa wanategemea kilimo cha
mboga mboga kujipatia kipato cha familia zao, ingawa wanakabiliwa na changamoto
ya kilimo duni kwani wanatumia nguvu nyingi na muda mrefu kulima kwenye eneo
dogo.
Amesisitiza kuwa, wakulima wanatakiwa kubadilika kwenda na wakati
kwa kutumia teknolojia mpya zikiwemo matumizi ya nishati ya jua ambayo inaweza
kuwasaidia kulima eneo kubwa na kupata kipato kikubwa.
Amesema, kuna wakulima wamekuwa wakichangia kununua jenereta
ambazo uendeshaji wake ni ghali ambapo mkulima hutumia lita tatu hadi tano kwa
kumwagilia ekari moja, na anaweza kutumia zaidi ya shilingi 400,000 kwa mwezi
kununua mafuta ambayo yamekuwa yakipanda kila siku.
“Ni kweli wakulima wamekuwa wakivutiwa na shamba langu
ambalo namwagilia kwa kutumia nishati jua, ni njia rahisi sana tofauti na
matumizi ya jenereta au mikono kwani ni kupoteza muda mwingi kwenye eneo dogo” amesema Dunia.
Ameongeza kuwa amekuwa akiwaelimisha wakulima kutumia
teknolojia hiyo ya nishati ya jua katika umwagilia lakini changamoto ni
mtaji wa kununua mitambo hiyo ambayo
inatofautiana bei kulingana na uwezo wa kumwagilia.
Diwani wa kata ya Shabaka Kharim Hamis Chasama anasema,
changamoto ya wakulima kukosa mtaji wa kununua nishati jua ipo lakini amewataka
kutumia fursa ya kuomba mkopo kwenye halmashauri kupitia mikopo inayotolewa na
serikali ili waweze kuhama kutoka kwenye teknolojia duni kwenda kwenye
teknolojia ya kisasa.
“Halmashauri ya Nyang`hwale imetenga kiasi cha zaidi ya
shilingi milioni 700 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa walemavu, vijana na
wanawake, hivyo wakiungana wakulima watano watano wakaomba mkopo wanaweza
kununua mitambo hiyo itakayowasaidia katika shughuli za umwagiliaji” anasema Chasama.
Akizungumzia teknolojia hiyo kaimu katibu tawala msaidizi
uchumi na uzalishaji mkoa wa Geita, Tito Mlelwa amesema kwa mkoa wa Geita kuna
maeneo matano yanayotumia kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya nishati ya jua.
“Matumizi ya pampu za kutumia mafuta ni ghali lakini
kiuhalisia matumizi ya pampu za nishati ya jua kuna faida kiuchumi na
kimazingira, na sisi kama serikali ya mkoa wa Geita tumekuwa tukiwahamasisha
wadau kwenda kwenye kilimo cha nishati ya jua” anasema Mlelwa.
Kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya umeme wa nishati ya jua
umenufaisha taasisi ya kilimo ya chuo kikuu cha kilimo Sokoine (SUA-SUGECO)
mkoani Morogoro inayotumia pampu za kusukuma maji kwa kutumia nishati ya jua.
Hivi karibuni katika mahojiani na waandishi wa habari
waliotembelea mradi huo kwa lengo la kujifunza teknolojia ya nishati ya jua, mkurugenzi
wake Dkt.Anna Temu alisema kilimo hicho kimeleta mapinduzi makubwa katika sekta
ya kilimo.
Aliongeza kuwa, taasisi hiyo imekuwa ikizalisha mazao mengi
kupitia kilimno hicho na kuuza mazao nje
ya nchi ikiwemo Dubai, tofauti na hapo awali walipokuwa wanamwagilia kwa jenereta
zinazotumia mafuta.
“Kwa siku tulikuwa tunatumia zaidi ya lita 50 kwa siku
kumwagilia shamba lililopo, lakini baada ya kuhama na kuanza kutumia nishati ya
jua uzalishaji mazao umekuwa mkubwa, tulitamani mkulima awe mkubwa” alisema Dkt. Anna.
Utafiti wa mwaka 2020 uliofanywa na Taasisi ya utafiti wa
maendeleo ya kilimo Tanzania (TARI) unaonyesha takribani asilimia 85 ya
wakulima wanaotumia Teknolojia ya umwagiliaji wanategemea pampu zinazotumia
mafuta ya dizeli ambayo ni ghali.
Kwa upande wa shirika la mendeleo la umoja wa Mataifa (UNDP)
mwaka 2021 lilibainisha kwamba kutumia pampu za umeme jua, wakulima wanaweza
kupunguza gharama za nishati kwa asilimia 70 hadi 80.
0 Comments